Breaking News

Thursday, November 22, 2012

HALIPOTOKA BANANA ZORRO

MAKALA NA ERICK EVARIST
“MAMA yangu, wewe ni nguzo maishani mwangu… taa imulikayo mbele yangu…” kilikuwa ni kiitikio cha wimbo ambao ulimpa heshima kubwa mwanamuziki mwenye sauti ya pekee Bongo, Banana Zahir Zorro.
 
Banana Zorro akiwa na watoto wake wawili, Landi na Jarmain.
HISTORIA YAKE KIFUPI
Banana alizaliwa mwaka 1983 huko mkoani Iringa. Baada ya kujitambua, wazazi wake walihamia jijini Dar. Akajiunga na Shule ya Msingi Kurasini tangu mwaka 1991 hadi 1997.
Mwaka 1998, alijiunga na Sekondari ya Mt. Methew ya jijini Dar, mwaka 2000 akahamia Metro Police hadi alipohitimu kidato cha nne mwaka 2001.
Banana (wa pili kushoto) akiwa na wenzake enzi hizo.
ALIANZIA WAPI MUZIKI?
Awali, Banana alikuwa akipenda kuiga kucheza staili za marehemu mwanamuziki kutoka nchini Marekani, Michael Jackson kabla hajajiunga rasmi kwenye kuimba baada ya kuhitimu kidato cha nne.
Aliichora ramani yake ya muziki pindi alipokuwa kidato cha pili. Alikuwa akiitumikia bendi iliyofahamika kama Bilovem, alipenyeza sauti yake kwenye wimbo wa bendi hiyo uliojulikana kama Anakudanganya na muda mchache baadaye walikamilisha albamu iliyobebwa na wimbo huo.
AJIUNGA NA IN AFRICA BAND
Harakati rasmi za muziki kwa Banana zilianza mwaka 2001, baada ya kuhitimu masomo ya sekondari. Alijiunga na bendi iliyofamika kama In Africa Band baada ya kuunganishwa na msanii mkongwe nchini, Bizman.
“Hapo tuliandaa albamu ya Indege ndipo nilipojifunza vyombo mbalimbali vya muziki,” anasema Banana.
MASHINDANO YA POP IDOL
Mwaka 2002, kupitia shindano kubwa la kusaka vipaji lililojulikana kama Pop Idol, Banana alishiriki na kupata daraja la pili na kuongeza umaarufu wake. Aliibuka kidedea kwenye mashindano hayo baada ya kuonesha uwezo wa hali ya juu wa kuimba.
 
Banana Zahir Zorro akiwa katika pozi.
ATOA ALBAMU YA KWANZA
Mkali huyo wa sauti, anasema nguvu zake kwenye muziki zilichanua baada ya kujizolea umaarufu mkubwa kwenye mashindano ya Pop Idol. Alifanikiwa kuachia albamu yake ya kwanza iliyojulikana kama Banana. Ilishiba nyimbo kali kama Mama, Wasiwasi na nyinginezo.
Moja kati ya matunda ya albamu hiyo aliyoitoa mwaka 2002 ni tuzo za Kilimanjaro 2003 kupitia kipengele cha Mwanamuziki Bora wa Kiume.
Milango ya ya shoo ikafunguka. Akaanza kufanya ziara mikoa karibu yote ya Tanzania akiwa na Mbongo Fleva, Q Chief na Papii Kocha ambaye ilikuwa wafanye naye wimbo wa pamoja. Ilishindikana baada ya Papii kufungwa.
AIKACHA IN AFRICA BAND
Mwaka 2005, Banana aliikacha Bendi ya In Africa. Akajikita katika muziki wa peke yake (solo artist), akafanikiwa kuingiza sokoni albamu yake ya pili iliyojulikana kama Subra.
Ndani ya albamu hiyo kulikuwa na vibao kama Mapenzi Gani, Mama Kumbena na Niko Radhi ambazo hadi leo bado zinafanya vizuri katika ulimwengu wa muziki ndani na nje ya Tanzania.
Kama ilivyokuwa katika albamu ya awali, ya pili nayo ilimuwezesha kujinyakulia tuzo mbili za Kilimanjaro Music Awards mwaka 2007. Alishinda katika kipengele cha Mwimbaji Bora wa Kiume pamoja na Wimbo Bora wa RnB (Niko Radhi).
AANZISHA BENDI YAKE
Mahesabu yake ya kuachia nyimbo kwa mpangilio maalum ndiyo yalimpa mafanikio kuweza kufikia malengo ya kuanzisha bendi yake iliyojulikana kama Banana Band au B. Band.
Banana akiwa na mkewe, Suzan siku ya ndoa yao.
AOA
Mwaka 2008, mkali huyo aliyetikisa na songi la Nzela alimuoa Suzan. Mpaka sasa amezaa naye watoto wawili, Landi ,6,  na Jarmaine ,4,. Baada ya hapo, ameendelea kurekodi nyimbo zaidi ya 35 ambazo hazijatoka mpaka sasa.
JE AMEFANIKIWA?
“Kiasi chake, kila siku napambana kusogea mbele zaidi. Kikubwa kwa sasa najivunia kuwa na bendi ambayo ina wafanyakazi 14 ambapo baadhi yao wanasomea muziki kutokana na kipato wanachokipata B. Band,” anasema Banana.
KWA HISANI YA GLOBALPUBLISHERS

No comments:

Designed By VungTauZ.Com