Breaking News

Wednesday, September 12, 2012

HARUSI YA MSANII WA BONGO MOVIE WILLIAM MTITU

Gladness Mallya, Dar es Salaam
YAANI we acha tu! Sherehe ya harusi ya msanii mkongwe wa filamu Bongo, William Mtitu imetia fora kutokana na matukio mbalimbali kwenye hafla hiyo, Risasi Mchanganyiko linashuka kifua mbele.
Mtitu alifunga ndoa na mkewe Yovina Swai, Jumamosi iliyopita katika Kanisa Katoliki, Parokia ya Mtakatifu Joseph, Posta jijini Dar es Salaam na baadaye kufuatiwa na sherehe ya kukata na shoka iliyochukua nafasi katika Ukumbi wa Urafiki, Ubungo, Dar.
WAONESHA TOFAUTI
Bwana na bibi harusi, badala ya kuingia na muziki wa taratibu kwa pamoja, waliingia huku wakikimbia, kila mmoja na njia yake halafu wakaanza kulisakata sebene jambo lililoamsha shangwe.
AUNT, WOLPER AIBU TUPU
Masistaduu wanaotesa kwenye ulingo wa filamu Bongo, Jacqueline Wolper na Aunt Ezekiel ndiyo walioongoza kwa mavazi yaliyotia aibu ukumbini.
Wolper alivaa gauni zuri lakini aliharibu kwa kuacha mwili wake wazi kuanzia juu kidogo ya kiuno hadi mabegani kwa kufunika na kijitambaa chepesi cha chekecheke (angalia picha ukusara wa nyuma).
Kwa upande wake Aunt alivaa kigauni kifupi ambapo alilazimika kukaa kwa shida huku akijitahidi kuficha ‘maeneo yake nyeti’ yasionekane, maana kila kitu kilibaki nje huku mabega yake nayo yakiwa wazi.
Mastaa wengine waliovalia magauni yenye mipasuo mikubwa hadi kufikia mapajani ni pamoja na Sabrina Rupia ‘Cathy’, Jenifer Kyaka ‘Odama’, Salama Salmin ‘Sandra’ na Shamsa Ford.
SAJUKI AACHA HISTORIA
Mwigizaji Sadick Juma Kilowoko ‘Sajuki’ ndiye aliyepewa jukumu la kutoa nasaha kwa maharusi, lakini katika hali isiyotarajiwa na wengi, alipita mbele akiwa ameshika kipaza sauti kilichokuwa kikitoa maneno ya kunadi sumu za kuulia wadudu.
“Sumu ya panya, mende, kunguni, viroboto...” jambo lililowachekesha sana wageni waalikwa.
DOSARI KIDOGO
Aidha kulitokea dosari kadhaa ukumbini humo; mosi, kutokana na udogo wa ukumbi na idadi kubwa ya watu, baadhi ya watu walikosa sehemu za kukaa hivyo kulazimika kusimama wakati wote wa sherehe hiyo huku wengine wakinong’ona kwamba vinywaji (vilevi) ni vichache na vinatolewa kwa kujibana.
“Kamati haikujipanga vizuri...sasa kwa nini walichukua ukumbi mdogo wakati wanajua wageni wao ni wengi hivi? Ona watu walivyosimama! Halafu vinywaji pia vinatolewa kiubabaishaji sana,” alisikika akisema mtu mmoja aliyekuwa jirani na paparazi wetu.

CHANZO:www.globalpublishers.info
Designed By VungTauZ.Com