Breaking News

Sunday, August 26, 2012

Rais Kagame aipa tano Yanga


RAIS Paul Kagame wa Rwanda, ameipongeza klabu ya Yanga kwa kutwaa mara ya pili mfululizo Kombe la Kagame na kusema mafanikio hayo yanatokana na umoja na mshikamano ndani ya klabu hiyo.

Kagame, ambaye ni mdhamini mkuu wa mashindano hayo, alikutana wachezaji wa Yanga na viongozi wao katika hafla aliyowaandalia kwa ajili ya kuwapongeza iliyofanyika Ikulu ya Kigali Jumatano usiku wiki hii.

Yanga ilitwaa ubingwa mara ya pili mfululizo baada ya kuifunga Azam FC 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa, ambapo mwaka jana ilifanya hivyo pia kwa kuifunga Simba 1-0 kwenye uwanja huohuo.

"Nawapongeza kwa ushindi wenu. Ni jambo zuri na inaonyesha ni jinsi gani mlivyo na umoja wa kweli katika michezo," alisema Kagame ambaye katika hafla hiyo uongozi wa Yanga ulimkabidhi jezi ya timu yao.

"Nataka kuwaambia neno moja, mafanikio mliyopata ni furaha kwa wote kwa maana sisi sote ni ndugu. Yanga ni klabu ya Tanzania na Afrika Mashariki, sisi sote ni wamoja.

"Nawaambieni, leo tunaweza kujiona sisi ni tofauti kwa sababu ya utaifa wetu, lakini akifuatilia chimbuko la wazee wetu wa zamani, utagundua sisi ni wamoja kutokana na mchanganyiko wetu," alifafanua.

"Kuna Watanzania wengi hapa Rwanda, lakini pia kuna Wanyarwanda wengi Tanzania. Hii inaonyesha ni jinsi gani tulivyo wamoja."

Wakati huohuo, Kocha wa Yanga, Thomas Saintfiet ameahidi kukirudisha kikosi chake mjini Kigali kupiga kambi baada ya kufurahishwa na mazingira ya mji huo.

Yanga imeweka kambi katika Hoteli ya La Pallise iliyopo eneo la Remera kujiandaa na michuano ya Ligi Kuu Bara inayotarajiwa kuanza baadaye mwezi ujao.

"Hii ni mara yangu ya kwanza kufika Rwanda, lakini hakika nimefurahishwa na mazingira ya hapa, naahidi nitarudi tena kuweka kambi na timu yangu," alisema Saintfiet mbele ya Rais Kagame.

"Nitafanya hivyo lakini pia huenda nikaleta tena kombe hili kwa mara nyingine kwa maana mazingira ni tulivu na mazuri, kila kitu kinaenda sawa,"alisema Saintifiet.

No comments:

Designed By VungTauZ.Com