
KARIBU nyumbani Bongo bidada Rehema Chalamila ‘Ray C’. Wewe ni mwanamuziki mkali wa Bongo Fleva na Zouk uliyezaliwa Mei 15, 1982 mkoani Iringa nchini Tanzania.
Hujaolewa lakini ulipotua nchini wiki iliyopita ukitokea Kenya ulipokuwa umeweka makazi, ulitoa vigezo vya mwanaume unayetaka akuoe, kuwa awe mtanashati na asiwe maarufu wala pedeshee. Safi kabisa, nakusifu kwa hilo japo umri unakutupa mkono. Una umri wa miaka 30 sasa lakini bado ni mrembo mwenye mvuto. Utambulisho unatosha.
Kama ulikuwa hujui, mimi ni mmoja wa watu waliokuwa wakihudhuria shoo zako wakati ule ukisifika kwa jina la Kiuno Bila Mfupa kutokana na kujua kukizungusha vizuri unapokuwa jukwaani. Shoo yako ya mwisho niliyokushuhudia jukwaani na ukafanya vizuri ni pale kwenye Viwanja vya Leaders Club, Kinondoni, Dar katika Kampeni ya Zinduka! Malaria Haikubaliki, mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, Februari 13, 2010. Acha kabisa, ulikonga nyoyo za watu. Kipo wapi kiuno bila mfupa mamito?
Tena nakukumbuka ulikuwa ukigonga shoo kubwakubwa za ndani na nje ya nchi kama China na Uingereza. Unakumbuka alipokuja mwanamuziki wa Marekani, Ja Rule ukapata nafasi ya kufanya naye shoo jukwaa moja? Connection na rapa huyo ziliishia wapi?
Ukashinda tuzo za muziki za Kili mara mbili ukiibuka kuwa Mwanamuziki Bora wa Kike mwaka 2004 na 2007. Mbali na hizo, ukajitwalia umalkia Afrika Mashariki, ukalamba zile za Kisima mwaka 2004. Ukateuliwa (nominated) kuwania zile za PAM mara tatu mwaka 2006, 2007 na 2008. Zimekwenda wapi zile tuzo mamito?
Inafahamika kuwa wewe ni miongoni mwa vijana watafutaji Bongo, hivyo kwa jina lako pekee, ulitakiwa uwe juu sana kimuziki, mshiko, majumba, mikoko mikali, kuibua vipaji na kurudisha fadhila kwa jamii kwa kujihusisha na uhamasishaji na kampeni mbalimbali kama ulivyofanya kwenye Zinduka! Malaria Haikubali.
Wakumbuke watu uliokuwa ukikimbizana nao kwenye gemu, sitaki kuwataja. Kama ulikuwa hujui, inawauma sana Watanzania hata kama unafanya vizuri huko kwa Rais Mwai Kibaki.
Ulipoanza kuyumba ni wakati ukiwa na uhusiano wa kimapenzi na rapa mkubwa Bongo wa Nako 2 Nako, Waziri Makuto ‘Lord Eyez’. Skendo zilikuwa ni nyingi, ikiwemo ile kubwa ya matumizi ya unga mweupe na sigara kubwa.
Ukagombana na media na matokeo yake ukatangaza kuokoka kabla ya kutimkia Kenya huku mama yako akikusihi kubaki nchini lakini ukawa sikio la kufa.
Kuteleza siyo kuanguka bidada! Pia yaliyopita si ndwele! Ukijiuliza maswali haya na ukapata majibu, ni rahisi kama kumsukuma mlevi kwa wewe kurudi kileleni kwenye gemu hapa Bongo.
Maswali yanayohitaji majibu ni je, uliteleza wapi? Je, mashabiki waliuchoka muziki wako hadi ukatimka nchini? Je, muziki unalipa zaidi Kenya? Je, hukutunga mashairi mazuri? Je, ulikosa sapoti ya wadau? Je, hukufanya promo (matangazo) ya muziki wako? Je, ulikosa shoo za kukuingizia kipato ili ujiendeleze? Je, kipaji kiliisha Bongo kikawa kinafanya kazi zaidi Kenya? Unahitaji vitu gani urejee kwenye muziki Bongo?
Come on! Kiuno Bila Mfupa, hivi unajua wewe ni madini? Rudi kwenye muziki wa Bongo bado unakuhitaji, ukizingatia wanawake mpo wachache kwenye gemu. Nimekuandikia kiroho safi kwani najua bado upo nchini kwa hiyo umenisoma. It’s for the love of game!
CHANZO: www.globalpublishers.info
No comments:
Post a Comment